Wacha Mungu wa Zama za Digitali
Wacha Mungu wa zama za digitali ni kitabu kinachoelezea mapinduzi makubwa ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) yanagusa maisha ya wacha Mungu kwa namna tofauti tofauti. Jambo hili linapelekea mabadiliko makubwa katika mawasiliano yanayolitishia Kanisa la Mungu na misingi yake. Namna watu wanavyowasiliana katika zama hizi za digitali kumeongeza kasi ya kubadilishana taarifa. Kasi hii ndiyo aliyoiona Daniel katika unabii wake wa zama za mwisho wa misingi ya dunia.
Shetani anatumia fursa hii ya haya maarifa makubwa kueneza uovu wake kwa kasi. Ili kutambua namna ya kujiweka salama katika zama hizi ni vyema kuzing’amua njia salama zinazopaswa kutumika wakati wa kufanya mawasiliano. Msingi wa matatizo yote ulimwenguni kwa asilimia 85% husababishwa na namna ya kuwasiliana.
Shetani alivyokuwa akiwasiliana na Eva katika bustani ya Edeni, alitumia mawasiliano vibaya na kufanikiwa kumhadaa Eva naye akamhadaa mume wake Adamu. Kwa kasi iliyo kubwa zaidi, Shetani aliye baba wa uongo ameendelea kutumia mapinduzi ya TEHAMA kwa namna ya upotofu ili kuangamiza roho yumkini hata za wateule wa Mungu.
Kitabu hiki ni maalum kwa ajili yako ili uweze kutambua changamoto ambazo unaweza kuzipata kama baba, mama au mtoto kutokana na matumizi ya Teknolojia Ya Habari Na Mawasiliano. Watu wengi wameumizwa na Mitandao kiasi wamejikuta wakibadili tabia au maadili yao.
Ufahamu mdogo wa mambo mengi unachangia sana mtu kufanya uchaguzi usio sahihi. Matumizi ya vitumizi vya mawasiliano vya kidigitali kama rununu, sikanu, tabiti, ngamizi na runinga yamekuwa yakiathiri sana mitindo ya maisha. Licha ya ukweli kwamba utamaduni hutoa miongozo mingi ya kimaisha bado kuna mambo ambayo hayapaswi kufanywa na wacha Mungu kwa sababu ya mapinduzi ya TEHAMA.
Maandiko Matakatifu yana nafasi kubwa sana ya kuonya na kuwaongoza wacha Mungu. Maana kila Neno la Mungu lafaa kwa mafundisho. Unapopata muda wa kuyachunguza Maandikio, tafakari pia mwenendo wako wa maisha. “Je, ni kwa kiasi gani simu yako imeyabadili maisha yako?” Maisha yameathirika kwa kiwango kikubwa katika nyanja ya mtu mmoja mmoja mpaka familia. Ni makosa gani umekuwa ukiyafanya kila siku kwa sababu ya kutumia simu? Ni wajibu wetu kuyatambua yale yanayotokea katika maisha yetu kama yanapaswa kufanywa au kuachwa. Ugunduzi wa maarifa makubwa ya mawasiliano unawagusa watu wote. Maarifa haya yamekuwa na athari chanya na hasi kwa wacha Mungu na wamejikuta wakiacha misingi ya imani zao.
Maudhui ya kitabu hiki ni kuwaonesha wacha Mungu njia salama za kuzingatia katika zama hizi za digitali ili maarifa haya makubwa ya mawasiliano yasipofushe ufahamu wao juu ya Mungu. Kupoteza kibali mbele za Mungu kwa sababu ya simu ni jambo la hatari na halipaswi kuachwa liwaangamize wacha Mungu.
Kuna baadhi ya maneno yametumika katika kitabu hiki yanaweza kuwa ni mageni kwako. Ili kuwa na uelewa mzuri wa kile kinachoelezwa ni vizuri ukasoma sehemu ya mwisho kabisa ya ‘Ufafanuzi wa Maneno’ kabla ya kuanza kusoma kitabu hiki. Sehemu hii itakupa tafsiri rahisi ya kila msamiati mpya uliotumika. Kwa kufanya hivyo utakuwa na nafasi nzuri zaidi ya kuelewa maudhui ya kitabu hiki. Lengo kubwa ni kuhakikisha kuwa wacha Mungu wanabakia salama licha ya matumizi yasiyo na staha yanayofanywa na watumiaji wengi wa vitumi vya mawasiliano vya kidigitali na mapinduzi yake.
Maisha ni kuchagua. Mungu alitupa uhuru wa kuchagua tangu mwanzo. Mbele yetu kuna uzima na mauti, chagua uzima ili umwone Mungu. Simu yako isije ikapelekea mauti yako na ya wale uwapendao. Jifunze njia sahihi za kukabiliana na mapinduzi ya TEHAMA katika zama za digitali kabla hujachelewa.
Simu, rununu, sikanu, tabiti, ngamizi, Mtandao na runinga ni vifaa tu vya mawasiliano. Isije ikatokea mtu anaikosa Mbingu mpya na Nchi ile mpya kwa sababu ya vifaa hivi. Hakikisha matumizi ya vifaa vya kidigitali hayakutengi na Mungu siku zote za uhai wako. Wala usikubali kuikosa Mbingu kwa sababu ya mawasiliano mabaya. Laiti ungelijua kile ambacho Yesu Kristo amekuandalia basi ungefanya bidii ili upate kumwona uso wake.
Ushindi katika maisha yetu tunaupata kupitia yeye maana alishaishinda dhambi msalabani. Licha ya uwepo wa zama za kutisha zenye ubinafsi mkubwa kutokana na kukua kwa maarifa bado watu wa Mungu wanapaswa kujipambanua katika mwonekano tofauti na wa ulimwengu hasa wanapozingatia kuwa huu ulimwengu ni wa kupita na makazi yao yapo Mbinguni.
Mungu ameahidi kuja kuishi na wanadamu katika mbingu mpya na nchi mpya. Mpango wake ni wa hakika. Hata hivyo ipo kazi ya kufanya kwa kuhakikisha ulimwengu na maarifa yake yote haukuangamizi milele. Mungu akubariki unaposoma kitabu hiki chenye wingi wa maarifa ya nyakati hizi.
YALIYOMO
➡ Shukrani…. 3
➡ Dibaji… 4
➡ Utangulizi … 5
➡ SURA YA KWANZA: Hofu Yangu …. 6
➡ SURA YA PILI: Mianzo Ya Mawasiliano… 15
➡ SURA YA TATU: Umuhimu Wa Mawasiliano… 37
➡ SURA YA NNE Dhana Potofu Kuhusu Mawasiliano… 48
➡ SURA YA TANO: Kero Za Rununu … 58
➡ SURA YA SITA: Changamoto Za Digitali Kwa Wacha Mungu… 69
➡ SURA YA SABA: Matumizi Salama Ya Vitumi Vya Mawasiliano … 145
➡ SURA YA NANE: Maadili Na Miiko Ya Teknolojia Ya Habari Na Mawasiliano… 189
➡ SURA YA TISA: Njozi Kwa Kanisa La Masalia… 208
➡ Ufahamu wa Maneno … 221
Onyo
Haki Zote Zimehifadhiwa. Huruhusiwi kutoa nakala ya kitabu hiki au sehemu ya kitabu hiki kwa sababu yoyote ile bila ruhusa ya mmliki wa kitabu kwa maandishi. Juhudi zimetumika kuandaa kitabu hiki kwa usahihi na umakini mkubwa sana kwa lengo la kutoa elimu na ujumbe ulio bora zaidi.
Ikithibitika kwa namna moja au nyingine umehusika kudurufu nakala au kusambaza katika mitandao ya kijamii na mingieyo nakala ya kitabu hiki utakuwa umetenda uharifu chini ya sheria ya makosa ya mtandao. Adhabu ya kifungu au faini au vyote kwa pamoja vinaweza kutolewa dhidi yako. Epuka wizi, kuwa mzalendo kwa kununua kazi za wasanii wetu. Wizi haukubaliki kiimani na hata kijamii.
Hata hivyo, taarifa, ujumbe au mafunzo yanayopatikana katika kitabu hiki hayana uhusiano wowote na matokeo ya msomaji. Mwandishi, mchapishaji au msambazaji hatawajibika kwa tatizo lolote litakalojitokeza kutokana na usomaji wa kitabu hiki.
Enock –
Superb
Juliana –
Mungu akubariki